Friday, February 14, 2014

KIUNGO Shomary Kapombe amegoma kurejea Ufaransa kwa madai halipwi mishahara, lakini AS Cannes imeitaka Simba SC itoe Euro 33,000 sawa na Sh. Milioni 66 ili irejeshewe mchezaji wake huyo.Ajabu sasa, mchezaji huyo anayeweza kucheza nafasi za ulinzi pia pembeni na katikati, alitolewa bure kwenda AS Cannes katikati ya mwaka jana akiwa bado ana Mkataba na klabu hiyo ya Msimbazi, unaomalizika Aprili mwaka huu.Amegoma; Shomary Kapombe amekataa kurejea UfaransaKatika mahojiano maalum na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe juu ya sakata la mchezaji huyo, ameiambia BIN ZUBEIRY  jana kwamba, Kapombe amewaangusha mno kwa kugoma kurudi Ulaya.“Mimi nilimuita Kapombe Desemba (mwaka jana) ofisini kwangu tukazungumza naye, akaniambia hataki kurudi Ufaransa kwa sababu wale jamaa hawakumpa mshahara wa Novemba, nikamuambia nenda watakupa kule, akagoma.Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe akiwa ameinua Kombe la Hisani, baada ya kuifunga Yanga 3-1 Desemba 21 mwaka jana katika mechi ya Nani Mtani Jembe.Nikamuambia kama suala ni hilo, mimi nakupa huo mshahara wako uende kule kama wale jamaa watanirudishia fedha zangu sawa, akakataa kupokea fedha. Pale pale nikajua kuna kitu kingine,”alisema Hans Poppe.Poppe amesema anaamini kabisa Kapombe amerubuniwa na timu moja ya nchini kati ya mbili, ili abaki hapa kujiunga nayo hivyo anatoa visingizio visivyo na mantiki.  Poppe amesema kwamba baada ya hapo, aliwasiliana na AS Cannes kuomba mchezaji huyo arejeshwe Simba SC, lakini wakaambiwa walipe Euro 33,000.“Hapa sasa ndio pagumu, sisi tulimtoa yule mchezaji  bure kwa makubaliano wakimuuza watupe asilimia 40, na kwa kweli Shomary angeuzwa pale, maana ile klabu inauza sana wachezaji na sisi tungenufaika kwa kupata fedha nyingi,”.“Na hili la sisi kulipa Euro 33,000 wakati pia mchezaji mwenyewe anamaliza Mkataba mwezi wa nne, inakuwa ngumu. Tulikuwa tuna sera nzuri sana kwa ajili ya kuwasaidia wachezaji, ila mambo yenyewe kama ndio hivi hatuwezi kufanya hivi siku nyingine,”alisema Poppe.Aidha, Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) amesema wameona bora waiache klabu hiyo ya Cannes imuuze Kapombe ili wao wapate asilimia yao 40 ya mauzo na dau wanalotaka ni Euro 70,000 sawa na Sh. Milioni 140,000 ambapo Simba itapata Euro 28,000 sawa na Sh. Milioni 56.Poppe amesema kwamba kwa kuwa Kapombe ana Mkataba na AS Cannes, basi klabu hiyo ndiyo itakayomuuza na anaamini watapata fungu lao.Hata hivyo, tayari Kapombe amefungua kesi Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) akiomba mkataba wake na klabu hiyo uvunjwe kwa sababu hawamlipi mishahara.Baada ya kuwa Ufaransa kwa zaidi ya miezi mitatu, Kapombe alirejea nchini Novemba mwaka jana kwa ruhusa maalum ya kuja kuichezea timu ya taifa katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Zimbabwe.  Baada ya mchezo huo, mchezaji huyo akaamua kubaki moja kwa moja nyumbani akidai halipwi mishahara.Mwisho wa mwezi Novemba ulimkuta Kapombe akiwa Tanzania na tangu hapo hajarejea tena Ufaransa, maana yake AS Cannes inaweza kumshinda mchezaji huyo katika kesi aliyofungua.


Posted via Blogaway

0 comments:

Post a Comment